Thursday, October 10, 2013

Sound of Soul itakuwa mitaani hivi karibuni


Sinema ni sanaa ya maigizo kwa njia ya vitendo, inayoelimisha jamii kwa mfumo wa picha. Lengo la mtayarishaji kutengeneza sinema ni kutaka kufikisha ujumbe kwa jamii iliyotuzunguka.
Wataalamu wa sanaa ya sinema, wamebainisha kwamba sinema imegawanyika katika makundi tofauti, kuna sinema zinazohusu maisha ya mtu fulani au famila. Sinema nyingine zinahusu jamii husika, mfano sinema ya Sound of Soul, inaelezea madhara ya tamaa katika jamii yetu ya kitanzania.
Kwa mujibu wa maelezo ya msemaji wa kampuni ya Swahili World Picture, Haji Dilunga
ambaye ndiye mtunzi na mwandishi wa script hiyo, amesema kisa hicho kiliwahi
kutokea miaka ya nyuma kabla ya yeye (Dilunga) hajazaliwa, baada ya kusimulia
aliamua kutayarisha sinema ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Dilunga ambaye ni mwandishi wa habari, amesema kisa hicho amekiboresha ili kiweze
kuwa na mvuto kwa watazamaji, pamoja na kuongeza matukio ya kusikitisha na
kuhuzunisha.
Amesema sinema hiyo inamzungumzia msichana Whitney, aliyekuwa na tamaa ya kutafuta
mali baada ya mali za urithi alizoachiwa na marehemu baba yake, kunyang'wa na Baba
yake mkubwa, alipokuwa na mdogo na hatimaye kufukuzwa kwenye nyumba yao pamoja na
mama yake.
Kitendo hicho kilimfanya Whitney kutafuta mali kwa udi na uvumba, ili aweze kuwa
na maisha mazuri. Kwa bahati nzuri alifanikiwa kuwa na maisha mazuri, baada ya
muda mfupi maisha mazuri yalimtumbukia nyongo.
Ni nani aliyesababisha maisha mazuri yamtumbukie nyonge, ni msichana mwingine
anayeitwa Lolita, Msichana huyu alitokea kumsumbua Whitney kupita kiasi. Nini
matokeo ya usumbufu wa Lolita kwa Whitney? Unajua kwanini alimsumbua? Jibu
utalipata baada ya kuangalia Sound of Soul.
Utamu wa sinema hiyo unakuja pale unapotaka kujua kama sio kufahamu, kilichompata
Baba yake mkubwa Whitney, baada ya kumnyang'anya mali Whitney. Alifanikiwa kutimia
mali hizo, au alizikimbia na kuchukuliwa na watu wengine? Ukibahatika kuangalia
Sound of Soul utafahamu kisa hicho cha kusisimua.
“Nadhani wale wanaofuatilia sinema ninazotengeneza, watakubaliana na mimi kwamba si bahatishi katika utunzi na uandishi wa script sambamba na kuidirect movie. Watakumbuka sinema zangu nilizoandika script na kudirect ni pamoja na Uwanja wa dhambi, I love you, Picnic, Bunge la Wachawi, Popobawa na Zindiko." Alisema Dilunga.
Sound of Soul inawataka vijana kutafuta mali au fedha kwa njia ya halali, pia wanatakiwa kufahamu kama umauti pia upo nyuma yetu. Kutafuta fedha au mali kwa njia zisizokubali na jamii yetu au muumba wetu, nikujitafutia matatizo katika maisha yako ya duniani na kesho ahera.

“Sisi ni tofauti na watengenezaji wengine wa sinema, sisi hatutengenezi sinema zenye visa vya mapenzi ya kufikirika. Tunatengeneza sinema zenye ujumbe wa visa vya kweli katika maisha ya binadamu." Alisema Dilunga.
Amesema Sinema kama uwanja wa dhambi ilivuma sana, mpaka leo bado watu wanaikumbuka. Kuna baadhi ya wapenzi wa sinema walitoka Mombasa kuja kuonana na waigizaji wa sinema ya uwanja wa dhambi.
“Hebu fikiri watu wamefunga safari toka Mombasa kuja Dar kuonana na waigizaji waliocheza uwanja wa dhambi, sio jambo la kawaida kutokea katika sanaa. Mara nyingi tumezoea kusikia na kuona watu wakitoka mikoani sio nje ya nchi." Alisema Dilunga.
Amesema Sound of Soul ni sinema nzuri inayofaa kuangalia na familia yako, kwa sababu imezingatia maadili ya kitanzania. Hakuna mwigizaji yoyote aliyevaa nguo za ajabu kama nusu uchi, unaweza kuangalia na watoto wako bila ya kujisikia vibaya.
Sinema hiyo imechezwa na Mwajuma Abdul Haji, aliyecheza kama Whitney. Fatuma Mwinchumu amecheza Mama Whitney, Jimmy Raphael amecheza kama Baba mkubwa. Nurati Ngereshi amecheza kama Lolita.
Wengine waliocheza majina ya kiuchezaji yakiwa kwenye mabano ni Zalka Athumani (Rose),Emilio John (Mganga Puchiro),Sikudhani Mkambo( Mke wa Puchiro), Clemencea Salum (Tina), Khadija Fundi(Bi Upupu), Peter Pascal (Mganga Chanuo),Apolinary Mathew(Bonzo) Abdullah Hassani (Bwino), Paul Leonard(Meneja), Amina Omary (Polisi), Paskazia Peter(Polisi), Halima(Magret),Yusuph (Polisi) na Said (Polisi)
Sound of Soul inatarajia kuingia sokoni mara baada ya kumalizika kueditiwa, kuna scene kama tatu zinafanyiwa marekebisho kwa ajili ya kuwapatia wapenzi uhondo wa aina yake.
Kwa wale vijana wanaotaka kuendeleza vipaji vyao, wanaweza kufika ukumbi wa CCM tawi la Amani siku ya jumanne, alhamisi na jumamosi saa kumi jioni. Au  wanaweza kupiga simu namba 0789 904 226 au 0657 675 531.

Thursday, July 18, 2013

Mama Kanumba kama mwanae kwenye filamu ya Without Daddy.

 
Ben Blanco,  Jamila na mwenzake katika Without Daddy
                                             Frola Mtegeo Mama yake Marehemu Kanumba
Mama wa aliyekuwa mwigizaji maarufu marehemu Steven Kanumba  maarufu kama Big Daddy,  Frola Mtegoa ameigiza filamu katika muendelezo wa kipaji cha mwanaye baada ya kuigiza katika filamu ya Without Daddy akishirikiana na watoto waliokuwa wakiigiza na marehemu Kanumba kama Patrick na Jamila, katika filamu hiyo mama Kanumba kaigiza katika kiwango cha juu.
Kwa mujibu ya maelezo ya  mkurugenzi wa kampuni ya Big Daddy Production, Irene Kaungwa amesema filamu ya Without Daddy ni kazi mwendelezo wa kazi ya marehemu Kanumba iliyotoka siku za nyuma ya Big Daddy na ni kazi ambayo imetengezwa kwa ubora wa kimataifa ikiwa sambamba na kumtambulisha mama Kanumba katika tasnia ya filamu Tanzania.
“Kampuni ya Big Daddy Production imekusudia kuleta mapinduzi makubwa katika tasnia ya filamu Tanzania, na katika kumuenzi marehemu tumemchukua mama yake na  kumshiriki katika filamu hii, nadhani umeona uwezo wa mama Kanumba. Naweza kusema ameonyesha uwezo mkubwa katika uigizaji na hii ni filamu yake ya kwanza,”anasema mkurugenzi.
Irene Kaungwa amesema stori ya sinema hiyo ametunga yeye, script imeandikwa na Haji Dilunga. Waigizaji waliocheza sinema hiyo ni pamoja Abdalah Mkumbilah ‘Muhogo mchungu’, Fatuma Makongoro ‘Bi. Mwenda’ Cathy Rupia, Mayasa Mrisho, ‘Maya’, Othuman Njaidi ‘Patrick’ Wastara Juma ‘Stara’ Abdul Ahmed ‘Ben Blanco’,  Patcho Mwamba na wasanii mahiri wengineo.


                         

Uru atamba amezaliwa kwa ajili muvi za mapenzi

                                                                           Uru Eke
Lagos, Nigeria
Mwigizaji wa sinema za Nigeria Uru Eke amesema anauwezo mkubwa wa kuigiza sinema za mapenzi, kwa sababu ana hisia kali za mapenzi. Hata hivyo amedai kwamba ameumbwa hivyo kuwa mkali wa kuigiza sinema za mapenzi.
"Nina uwezo mkubwa wa kuigiza aina hizo za filamu za mapenzi kwa sababu nimezaliwa nikiwa ni mtu mwenye hisia kali katika mapenzi," alisema mwigizaji huyo anayekuja juu kwa sasa na kutamba kwamba mwigizaji, Ramsey ni miongoni mwa waigizaji wa kiume wenye hisia kali katika mapenzi. Angependa kucheza naye kama angeambia kuchagua mwanaume wa kucheza naye sinema za mapenzi.
Licha ya kusema hivyo amesisitiza kwamba hisia zao za mapenzi zitakuwa katika kuigiza baada ya kuigiza hakuna kitakachoendelea.
" Najua kama Ramsey Noah ni mume wa mtu, kwa hivyo hakuna kitakachoendelea zaidi ya kuigiza na kila mtu kuendelea na shughuli zake," alisema Uru Eke aliyezaliwa London na kupata elimu ya msingi London. Elimu yake ya sekondary alipata Nigeria, baada ya kumaliza elimu ya sekondari alikwenda Uingereza kupata elimu ya chuo katika chuo cha City University.

Sura ya Van Vicker yapagawisha mademu

                                                                      
                                       Van Vicker akiwa na mkewe pamoja na watoto zao
Lagos, Nigeria
Licha ya kupewa heshima kubwa ya kushiriki katika mambo mbali mbali ya kijamii ya ndani na nje ya nchini ya Ghana, mwigizaji maarufu katika anga la sinema za kiafrika. Mghana Van Vicker ametokea kuwa kivutio kikubwa kwa mademu kutokana na sura yake nzuri aliyojaaliwa na mwenyezi mungu.
Mghana ametokea kuwachengua waigizaji wenzake wa kike mpaka mashabiki wanaoangalia sinema zake.
Hata hivyo mwenyewe anadai kilichompeleka Nigeria ni kazi sio mademu. Van Vicker amefanya kweli katika sinema ya Beyonce - The President daughter. 

Chioma Toplis amemaliza bifu lake na Oge Okoye

                                                                 
                                                             Chiamo Toplis
                                                                               
                                                                       Oge Okoye

Lagos, Nigeria
Mwigizaji nyota wa Nigeria Chioma Tolips ametangaza hadharani kuwa hana tena ugomvi kama sio bifu na mwigizaji mwenzake anayejulikana kwa jina Oge Okoye. Bifu hilo lilikuwa la muda mrefu, hivi sasa ameamua kuachana na bifu na kujikita zaidi kwenye biashara zake.
Chioma alizungumza hivyo baada ya kuulizwa na mtandao mmoja wa taariza za sinema za kinaigeria, kuhusiana na bifu hilo kwani lilikuwa gumzo katika vyombo mbali mbali vya habari nchini Nigeria kwa kipindi kirefu.
Kwa mujibu wa maelezo yake Chioma amesema amewasamehe watu wote waliomfanyia mabaya, akiwemo  Oge Okoye ambaye alisumbuana naye kwa muda mrefu.
" Ukweli ni kwamba siwezi kuongea chochote kuhusu Oge kwani, nimemsamehe kutoka moyoni. Tena si yeye tu hata waengine waliowahji kuniendea kinyume,"alisema Chioma mwanadada mwenye umbo kubwa la kuvutia.
Hata hivyo amedai kwamba kilichotokea ni kama darasa, yaani amejifunza kutokana na tatizo hilo, hivi anaendelea na shughuli zake.


Danny Schechter ameitangaza Tanzania kwenye Movie ya Mandela

                                                                              
                                                                     Danny Schechter
Danny Schechter  a.k.a The News Dissector kwa wale wasio mfahamu ni mtayarishaji  kama sio mtengenezaji wa sinema ya Nelson Mandela – “Countdown to Freedom” na “Mandela in America” ametaka dunia kuiheshimu Tanzania kwa nafasi yake kubwa kwenye kutengeneza demokrasia Afrika Kusini.
Schechter anayefanya dokumentari ya utengenezaji wa filamu ya Long Walk to Freedom kama alivyotakiwa na Nelson Mandela mwenyewe, alisema Tanzania ilitoa ushirikiano mkubwa kukomboa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Afrika Kusini.
Jumapili katika Tamasha la ZIFF ilikuwa ni siku ya kuangalia Afrika Kusini kabla na baada ya Uhuru. ZIFF iliweka siku maalumu ya Afrika Kusini kutokana na maendeleo ya hali ya afya ya Nelson Mandela ambayo sasa inazungumzwa duniani kote.
Mandela ambaye katika dokumentari hiyo anaonekana akifafanua vitu mbalimbali, alielezwa na Schechter kama mtu maarufu ambaye hakutaka kuitwa mtakatifu pamoja na kwamba aliombwa kutengenezewa sanamu na kuwataka wasifanye hivyo na badala yake kusaidia ujenzi wa zahanati.
Alisema dunia inapaswa kutambua kwamba katika ukombozi wa Afrika Kusini, Tanzania ni nchi muhimu ingawa dunia inaonekana kutotambua hilo lakini wenyewe wa Afrika Kusini wanafahamu.
Alisema baada ya kuwapo na nia ya kutengeneza filamu yake, Madiba alimwandikia barua ya kumtaka kutengeneza dokumentari inayohusu utengenezaji huo kwa kuhakikisha ukweli uliopo kama unazingatiwa.
Alisema hali hiyo ilimfanya kufika Tanzania japo alishawahi kufika wakati wa harakati za ukombozi. Schechte ambaye ni mwandishi wa habari za uchunguzi, mtengeneza sinema huru, bloga na mhakiki vyombo vya habari, alisema ni vyema dunia ikatambua mchango wa Tanzania kwa ukombozi si wa Afrika Kusini, bali na mataifa mengine ya Afrika.
Alisema pamoja na utawala wa Makaburu kuzishambulia nchi zilizokuwa zinasaidia ANC kama Zimbabwe, Msumbiji, Angola na Zambia, ilishindwa kufanya hivyo kwa Tanzania ambayo licha ya kuwa na makambi ya mazoezi ya kivita, pia ilikuwa na shule za kufunza viongozi wa baadaye wa Afrika Kusini, Morogoro.
Dukumentari hiyo yenye tofauti kubwa na zile zinaozotengenezwa kwa ajili ya kuoneshwa katika televisheni, inamweleza Mandela kama mtu wa watu huku waliohojiwa wakielezea matumaini na nini kinafanyika.

Sunday, July 14, 2013

Beckham kuigiza nafasi ya James Bond

                                                                   
                                                                      David  Beckham

London, England  
Mke wa aliyekuwa mwanasoka wa Klabu ya Manchester United, Victoria Beckham amependekeza jina la mumewe, David Beckham kuwa miongoni mwa majina yatakayochaguliwa kupata nafasi ya kuigiza kama James Bond katika mfululizo wa sinema za 007, zinazomtumia muhusika mkuu anayeitwa James Bond.
Mapendezo hayo yanafanyika baada ya mwigizaji, Daniel Craig anayecheza sasa kama James Bond kubwaga manyanga. Majina yaliyopendekezwa ni kucheza kama James Bond ni pamoja na Christian Bale, Henry Cavill, Tom Hardy na Idris Elba.
Victoria ana amini Beckham anaweza kuitendea haki nafasi hiyo kuliko wote waliotaja kuziba pengo la Daniel Craig anayeacha kucheza nafasi hiyo.
" Nina uhakika Beckham ni bidhaa inayouzika, kama watamtumia kucheza kama James Bond. Sinema hayo itapendwa na watu wengi sana hata wale ambao sio mashabiki wa kuangalia sinema, kwa sababu Beckham ni mtu wa watu," alisisitiza Victoria alipokuwa anaongea.
Kama watampa nafasi ya kucheza kama James Bond, Beckham atafanya vizuri, kwanza ni mwanaume mwenye mvuto. Sura yake nzuri na shepu ya umbo lake ni nzuri tofauti na wanaume. Kwa hiyo watu watapenda kumtazama.
Hata hivyo Beckham mwenyewe alipoulizwa, alisema hana uhakika kama ataweza kufanya vizuri, kwa sababu hajawahi kuigiza au kusimama mbele ya camera kuigiza.
"Sina uhakika kama nitakuwa mzuri katika kuigiza, kwa sababu sijawahi kufanya kitu kama hicho katika maisha yangu. Ila kama nitapewa nafasi naweza kufanya. Nina rafiki yangu Tom Cruise ambaye ni mwigizaji mkubwa, labda ninaweza kuwa kama yeye. Ila sijafikiria kitu kama hicho kwa sasa," alisema Beckham, wengi wanamkumbuka kwa uhodari wake uwanjani.

Demi More kuacha kuigiza sinema

                                                                          Demi More
 Mwigizaji maarufu duninia mwanadada Demi More anafikiria kuacha kuigiza na kufanya kazi ya kufundisha mazoezi ya ya viungo maarufu kama yoga. Demi amefikia hatua hiyo baada ya kupigwa talaka na aliyekuwa mume wake.
Mwanadada huyo alipigwa talaka baada ya kukubali mwenye bila ya kulazimishwa kama alikuwa na tabia ya  kutoka nje ya ndoa yake.


Anayenitaka kufanya kazi aje Mbeya- Kinyembe

                                                                            Kinyembe
Komediani anayetamba kwa kubadilisha sura na sauti yake katika filamu za uchekeshaji anazocheza, Mohamed Abdallah a.k.a Kinyembe amesema licha ya kuisha na kuigiza Dar lakini anapenda kuishi mkoa kwake Mbeya.
Amesema kumekuwa na tabia ya waigizaji wengi wakifanikiwa kupata majina makubwa wanahama mikoani na kuja kuishi Dar.
Yoyote anayetaka kufanya kazi na  Kinyembe hana budi kufunga safari mpaka Mbeya kwa ajili ya kufanya naye. Ni mwigizaji anayeonekana kwa sana katika michezo ya vituko show kupitia televisheni ya Channel Ten.

Snura Mushi kuibuka ndani muvi mpya

                                                                        Snura Mushi
Mwigizaji wa kike na mwimbaji wa muziki wenye midundo ya kipwani yaani mduara, Snura Mushi aliyetamba sana katika tamthilia ya Jumba la dhahabu na sinema mbali mbali, amefunguka na kudai kwamba muziki umempa dili la kwenda kurekodi filamu Afrika ya kusini.
Amesema watayarishaji wa sinama ya Tandeka iliyorekodiwa jijini Pretoria, walimshirikisha kutokana na kufanya vizuri kwa wimbo wake wa Majanga. katika sinema hiyo ametumia lugfha ya kiswahili, kizulu na kiingereza.

Gari ya Mercy imeandika Odi's wife badala namba

                                                                     Mercy Johnson
Lagos, Nigeria
Mwigizaji maarufu wa Nigeria, Mercy Johnson, nyota inaonyesha bado inaendelea kung'ara baada ya kuendelea kupokea zawadi mbali mbali toka kwa mumewe, baada ya kujifungua salama na kurejea nchini toka Marekani alikokwenda kujifungua.
Baada ya kurejea nchini, amekuwa akipokea zawadi bandika bandua toka kwa mumewe Odi Okojie.
Licha ya kumnunulia nyumba kwa ajili ya familia yake, amemnunulia gari ya kifahari aina SUV kwa ajili ya matembezi ya kawaida. Gari hiyo badala ya kuandikwa namba kwenye kibao cha namba, imendikwa maneno yanayosomeka kama Odi's wife ikimanisha mke wa Odi Okojie.Hayo ndiyo maisha ya mastaa wa kinigeria.

Dokii ana upeo mkubwa wa kubuni katika sanaa

                                                                     
                                                                    Dokii  katika pozi
                                                                   Dokii akiwa jukwaani

Mwigizaji mjanja na wa kulenga na hatimaye kufanikiwa katika kila anachotarajia kufanya, Dokii amesema alikuwa mwanamuziki wa kwanza kufikiria kutunga na kuimba wimbo wa kumkaribisha rais wa Marekani Barack Obama aliyetembele nchini.
Ni wanamuziki wachache wenye upeo na ufahamu kutunga na maisha yanayoendana na matukio uhusika.
Kwa mujibu wa maelezo yake mbali ya kutunga na kuimba  wa kumkaribisha Obama, pia anatarajia kutayarisha sinema itayozungumzia safari ya Obama nchini.

Sipendi rafiki mnafiki- Yvonne Nelson

                                                                      Yvonne Nelson
 Lagos, Nigeria
Mwigizaji maarufu wa Nigeria, Yvonne Nelson amesema anachukizwa na marafiki wa wanafiki, amesema hapendi marafiki kama hao wanaochukua taarifa zake za siri na kuziandika kwenye blog.
Yvonne ambaye hivi karibuni alifanyiwa kitu mbaya na rafiki yake wa karibu, kitendo kilichomchukiza na kufikia kudai kwamba rafiki wa aina hiyo ni sawa na mchawi.
"Kama rafiki yangu ni lazima atafahamu mambo yangu ya siri, kufahamu siri zangu isiwe sababu ya kuandika katika blog. Binafsi nakerwa na marafiki wa aina hiyo, nitakuwa makini nao," alisema.

Sitaki wanaume wenye fedha- Jacqueline Wolper

                                                                  Jacqueline Wolper
Mwigizaji wenye aliyeshinda tuzo ya mwanamke mwenye mvuto  Jacqueline Wolper amesema hawapendi wanaume wenye fedha kwani wengi wao ni wanaume za wanawake wengine sio rahisi kuonyesha mapenzi yao ya dhati kwake, pia hawezi kutembea nao hadharani kwa kuhofia ndoa zao.
"Unajua unapokuwa na mwanaume mwenye fedha wakati ni mume wa mwanamke mwingine, hamtaweza kutembea pamoja, lakini ukiwa na kijana mwanzako hata kama hana fedha mtaweza kuongozana na kufurahia mapenzi wenu," alidai Diva huyo mwenye macho ya mvuto, sio kwa wanaume hata wanawake wenzake wametokea kumpenda.

Meagan Good atetea kivazi chake alichovaa BET

                                          
                                                           Meagan  katika vazi linalolamikiwa

                                                            Meagan  katika vazi linalolamikiwa
Los Angeles, Marekani.

Mwigizaji maarufu, Meagan Good alitoa mpya baada ya kutinga katika utoaji wa tuzo za BET, baada ya kuvaa kivazi kinachoonyesha sehemu kubwa ya mwili wake ukiwa wazi.
Meagan amabye siku hiyo alivaa gauni la bluu lililoacha wazi sehemu kubwa ya mwili wake ukiwa wazi hasa sehemu ya kifua.
" Mimi sio mtakatifu, lakini pia gauni lile halinifanyi kuwa shetani ni nguo ambayo niliipenda na kuamua kuivaa siku ile ya Tuzo za BET," alisema Meagan.
Hata hivyo, utetezi huo umeongeza moto wa majadiliano, watu wakidai kwamba yeye ni mke wa mchungaji hakupaswa kuvaa gauni la aina hiyo.

Sinema yangu ya Safari itachukua Tuzo- Richie

                                                                    
                                                                  Single Mtambalike
Nyota wa sinema za kitanzania, mkongwe Single Mtambalike maarufu kama Richie ametamba kuchukua tuzo kupitia sinema yake mpya ya Safari.
"Nimetayarisha sinema ya Safari kwa umakini, hivyo ni lazima iwe filamu ya kuingia katika tuzo mwaka huu kulingana na ubora wake, hata wasanii walioigiza wameigiza kwa kiwango cha juu," alitamba Richie.
Mkongwe huyo anadai kuwa yeye ni bora kwani ndiye msanii wa kwanza kabisa Tanzania kupewa tuzo na M-net mwaka 2006 huku akisifia utaratibu uliotumika kupatikana mshindi katika tuzo hizo.

Stephanie Okereke amepata tuzo

                                                                   
                                                                 Stephanie Okereke                                                      
Lagas, Nigeria
Diva wa sinema za Nigeria, Stephanie Okereke amepata tuzo maalumu baada ya kuigiza filamu inayofahamika kama Dry. Sinema hiyo inazungumzia masuala yanayohusiana na ugonjwa wa FISTULA.
Kwa mujibu wa waliotoa tuzo hiyo, wamesema sinema hiyo ni miongoni mwa sinema bora zaidi hasa ukizingatia namna ilivyochezwa na kuelezea tatizo la ugonjwa wa FISTULA.
" Ni sinema nzuri inayoelezea namna ya kinamama wanavyokumbana na tatizo la kutokwa na haja ndogo kiholela."
Tatizo limekuwa likiwaweka njia panda wanawake wengi kwa sababu hana elimu ya kupata ufumbuzi wa tatizo na hawajui kinga ya tatizo hilo. Sinema hiyo imetoa mwanga kwa kueleza namna ya kukabiliana na FISTULA.Juhudi binafsi zilizoonyeshwa na mwigizaji huyo zimemsaidia kupata tuzo hiyo.

Jacob Stephen .a.k.a JB amebeba ubalozi wa Oxfam


                                                                       Jacob Stephen
Mwigizaji nyota wa sinema za kibongo, Jacob Stephen maarufu kama kwa jina la JB, amechaguliwa kuwa Balozi wa Oxfam katika kampeni inayoitwa Grow.
" Nashukuru kupewa nafsi ya bolazi wa Oxfam kazi ambayo nimekuwa nikiifikiria siku zote, inahusu kuwasaidia weye matatizo ya chakula hasa watoto,"alisema JB anayetamba katika tasnia ya sinema hivi sasa, na kuwafunika waigizaji wengi wa kiume kwa kuigiza kwa kiwango cha hali ya juu. Amefanikiwa kuwa kipenzi cha watoto.




Saturday, July 13, 2013

Najivunia uwezo wangu wa kukata viuno- Shilole


                                                                       
                                                             Shilole katika pozi la nguvu
                                                                             Shilole

Mwanadada mrembo na mwigizaji maarufu katika tasni ya sinema za kibongo, Zuwena Mohamed a.k.a Shilole ambaye hivi sasa amejikita katika muziki, na kufanikia kutamba na kutishia waimbaji wa kike wenye uwezo, nyimbo zake zimetokea kupendwa na kufanya vizuri.
Wengi hawakutegemea kama angweza kufanya vizuri katika soko la muziki, kwani kuna baadhi ya waigizaji waliojaribu kuimba kama vile Zerishi, mwigizaji aliyetamba katika sinema ya Ngome ya Mwanamalundi.
Kwa Shilole hali imekuwa tofauti, ameweza kujipata umaarufu mkubwa na kupata maonyesho mengi.
"Ninapata maonyesho mengi kwa sababu ninapokuwa jukwaani, najituma kadri ya uwezo wangu kucheka, yaani kukata viuno. Najivunia uwezo wangu wa kukata viuno." alitamba Shilole msichana mwenye umbo la kuvutia na kuhamasisha kwa kila nguo anayovaa kwa inampendeza.
Nyimbo yake ya Paka la Baa iliyokuwa katika mtindo wa mduara, imejipata umaarufu kutokana na mashairi yake kugusa maisha ya halisi ya baadhi ya watu wenye tabia ya zisizokubali na jamii.
Kama kawaida yake anawashukuru wapenzi na mashabiki wake kwa kumkubali,pia amewataka waendelee kumpa sapoti kwa kuzikubali kazi nyingine anazotarajia kutoa hivi karibuni.
Shilole ameweza kufanikiwa kuwasisimua mashabiki wake, wanawake na wanaume kwa uwezo wake wa kuzungusha kiuno.
Zamani kabla ya Shilole  alikuwa akisifiwa Ray C kwa kuzungusha kiuno mpaka akapachikwa jina la kiuno si mfupa.




Auntie Ezekiel aibuka kwenye bongo fleva

                                                   Auntie Ezekiel katika moja ya pozi lake
                                                    Auntie Ezekiel katika  pozi jingine

Baada ya kujipatia umaarufu mkubwa katika uigizaji, mwanadada nguli katika uigizaji wa sinema za kibongo, Auntie Ezekiel ameamua kujikita katika muziki, baada ya kushirikishwa kwenye wimbo unaoitwa Movie Star wa January Joseph a.k.a January Eleven.
Kwa mujibu wa maelezo yake, Auntie Ezekiel amesema ana mambo mengi anayotaka kufanya katika muziki, ila kwa sasa hajawa tayari kuweka wazi mambo hayo. Ila anasubiri kuona namna mashabiki watakavyompokea.
"Nimeamua kuwaonyesha mashabiki na wapenzi wangu kwamba ninaweza kufanya muziki, kama nikubalika nitaamua kujiingiza moja kwa moja kwenye muziki. Ila naamini kama nitapokewa vizuri na kukubakli," alisema nyota huyo wa sinema ya Sound of death.
Kama Auntie Ezekiel ataingia moja kwa moja katika muziki, atakuwa anaungana na waigizaji wengine walioamua kujiingiza kwenye muziki kama vile Zuwena Mohamed maarufu kama Shilole, Salma Jabu maarufu kama Nisha, Flora Mvungi na Snura Mushi. 

Vyombo vya habari vilinikosea- Ini Edo

                                                                            Ini Edu
LAGOS, Nigeria
Nyota wa sinema za Nigeria anayeongoza kwa utajiri, Ini Edo amesema skendo pekee iliyowahi kumchukiza katika maisha yake ni ile iliyoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari, ikimuhusisha na uvutaji wa dawa za kulevya.
Amesema vyombo vya habari vilimkosea kwa kuandika habari ya uzushi, habari ambayo ilinivunjia heshima yangu kwenye familia, marafiki, mashabiki na wapenzi wangu wa ndani ya Nigeria na nje.
" Skendo ile ilinipa wakati mgumu sana, ila nashukuru wapenzi na mashabiki zangu, waligundua ukweli kama sio mtumiaji wa madawa ya kulevya. Skendo ile iliandaliwa na wabaya wangu kwa lengo la kunishusha kiugizaji."
Alipoulizwa kama anavuta sigara, mwanadada mwenye mvuto wa kimapenzi, alisema amekuwa akifanya hivyo katika baadhi ya filamu alizocheza, lakini kwa kawaida si mvutaji wa sigara na hataraji kuvuta katika maisha yake.
Ini alidai mtazamo wake ni tofauti na wasichana wengine wanaodai kuzaa kunaharibu shepu ya mwanamke, amesema sio kweli. Kwa sababu mwanamke aliyeolewa, kuzaa ni jambo la lazima na kwamba anapenda kuwa na watoto
“Sihofuu kupoteza umbile langu kwa sababu ya kuzaa. Wakati utakapofika, nitaanza kuzaa. Napenda watoto. Siwezi kusubiri muda mrefu kupata watoto,”alisema mwanadada huyo mwenye umbo na sura yenye mvuto alipohojiwa hivi karibuni.
Hata hivyo, Ini amesema kama ni uzuri, alikuwa nao alipokuwa na umri mdogo. Alisema aliziona baadhi ya picha zake alipokuwa mdogo na kuvutiwa nazo kiasi cha kumfanya kutoa amani kama ni yeye.
Ini alisema hana njia yoyote anayoifanya ili aonekane mrembo zaidi ya kufanyakazi zake kwa bidii, kula vizuri, kuiweka ngozi yake katika hali nzuri na kuwa mwenye furaha muda wote.
Mwanadada huyo alisema anamshukuru Mungu kwamba maisha yake ya ndoa yanakwenda vizuri na kuongeza kuwa, kwa sasa ameamua kuacha kuigiza nafasi, ambazo zinaweza kuitia doa ndoa yake.
Alisema kamwe hajawahi kuigiza filamu za ngono na hawezi kufanya kitu kama hicho katika maisha yake yote. Alisema anapenda zaidi kuigiza filamu zinazoelezea maisha halisi ya jamii kwa vile ndizo zinazokuwa na mvuto zaidi kwa jamii.
Mwanadada huyo mwenye macho ya mwito alikataa kutaja kiasi cha pesa, ambacho amekuwa akilipwa katika uigizaji wa filamu. Hata hivyo, alikiri kwamba amekuwa akilipwa fedha nyingi.
Ini alikiri kuwa si rahisi kumudu kuwa mke wa mtu na mwigizaji. Alisema anajitahidi kadri ya uwezo wake kumudu mambo hayo mawili na kwa kiasi fulani amefanikiwa.
“Nimekuwa nikipanga mapema ni lini niwe mahali fulani na lini nisiwe mahali hapo. Siweki vitu vingi kwenye sahani moja kwa wakati mmoja kwa sababu nikifanya hivyo, nitashindwa kufanya vitu vingine wakati ninapaswa kuvifanya. Bado nafanya kila kitu ambacho mwanamke anapaswa kukifanya. Kila ninapotoka kazini, nafanyakazi ya kupika nyumbani,”alisema.
Ini, ambaye ni msomi wa shahada ya sanaa alisema iwapo asingekuwa mwigizaji, angependa kuwa mwanasheria au mwanahabari.
Hata hivyo, Ini alisema upo uwezekano pia angeweza kufanyakazi nyingine yoyote ilimradi tu awe anaipenda.
“Mimi ni mtu makini katika kila jambo. Kila kitu ninachokiseti kukifanya katika akili yangu, kama ninakipenda, lazima nikifanye,”alisema.
Hivi karibuni, Ini alizindua filamu yake mpya ya I Will Take My Chances, ambayo Ini ameielezea kuwa, ana hakika itafanya vizuri sokoni na kupendwa na mashabiki.
Ini alisema ilimchukua miezi miwili kutengeneza filamu hiyo, mwezi mmoja kwa ajili ya mazoezi na mwezi mwingine kwa ajili ya kupiga picha za filamu hiyo.
Mwanadada huyo alisema licha ya kuolewa, hafikirii kustaafu kucheza filamu kwa sasa na kwamba hakuna kinachoweza kumfanya afikie uamuzi huo.
Alisema kwake, uigizaji wa filamu hautokani na kutafuta pesa, bali mapenzi kwa kazi hiyo.
Mumewe Ini kwa sasa anaishi nchini Marekani. Lakini mwanadada huyo amesisitiza kuwa, hilo si tatizo kwao kwa sababu wamekuwa wakikutana mara kwa mara.
Katika kujiweka safi kimwili, Ini amesema siku zote amekuwa akipenda kusafisha uso wake na kuuweka safi. Alisema anapokuwa hana kazi ama tukio lolote, hatumii vipodozi kutengeneza uso wake.

Nikifa sitaki nikumbukwe kama mwigizaji- Eucharia




                                                             Eucharia Anunobi Ekwu
Lagos, Nigeria
Mwanamama nyota wa sinema za Nollywood Eucharia Anunobi Ekwu  ameachana na uchezaji wa sinema na kuamua kuokoka, kumtumikia mungu kwa muda wa maisha yake yaliyobaki hapa duniani.
Hivi karibuni  Euchari alitangaza kuachana na uigizaji na kuamua kumrudia mungu kwa kuokoka baada ya kutamba kwa sana katika sinema nyingi alizoshiriki kuigiza.
Katika mahojiano yake na kituo kimoja cha televisheni cha hapa Nigeria, Eucharia amesema  akifariki dunia akumbukwe kama aliwahi kuwa mwigizaji wa sinema.
"Ingawa nimecheza muvi nyingi kwa muda mrefu, lakini nasema wazi kwamba, nikifa nsikumbukwe kama msanii bali ni mtu wa mungu ambaye nimeamua kumtumikiakwa kipindi cha maisha yangu yote yaliyobaki duninai,"alisema mwanadada huyo mwenye mvuta wa kimapenzi na macho ya kuita.
Euchari atakumbukwa na wapenzi na mashabiki katika sinema ya Abuja Connection, sinema hiyo ameshirikiana kuigiza na wakali wengine kama Clarion Chukwura Abiola, Ngozi Ezeonu, Chidi Mokeme Enabeli Elabuwa na wengine wengi wenye majina makubwa Nigeria.
Sinema ilitungwa na Ojiofor Ezeanyaeche, script iliandikwa na Adim Williams sambamba na kuongozwa na Adim Williams mwenyewe.

Lindsay mrembo mwenye matumizi mabaya fedha


                                                                   Lindsay  Lohan
                                                                      Lindsay Lohan
New York, Marekani
Mwigizaji, Lindsay Lohan ni miongoni mwa warembo waliokuwa katika chati ya juu kwa kuvuta hisia  za wengi kutokana na muonekana wake sambamba na vituko vyake, anavyofanya kila kukicha.
Mwanadada huyo anayependa kutumia fedha vibaya kama vile ameokoa, wakati ni fedha zake alizopata kwa kufanya kazi usiku na mchana. Jarida la Forbes la mwaka jana, limeandika kwamba Lindsay ameshika namba thalethini katika orodha ya waigizaji wanaotafuta fedha ili waweze kuishi maisha mazuri.
Lindsay mwenye umri wa miaka 27  raia wa Marekani ana utajiri wa dola 11 milioni.Utajiri huo umetokana na uigizaji, uimbaji wa muziki, uanamitindo na utangazaji wa manukato.
Kutokana na matumizi yake kuwa mabaya, mwaka 2011 alijikuta akifikia hatua ya kufilisika, mahesabu ya haraka aliyofikia ili aweze kupata fedha, ni kupiga picha za utupu na kupata dola milioni moja. Baada ya kupiga picha hizo alipata fedha na kurudi tena kwenye chati ya wenye fedha.
Kwa kutaka kuonyesha jeuri ya fedha alipangisha nyumba kwa dola 10,000 kwa mwezi. Anatumia dola 800 kila wiki kwa ajili  ya kutengeneza nywele zake, alinunua gari aina porsche kwa dola 80,000.
Amekamatwa mara nyingi kuhusiana na utumiaji wa madawa ya kulevya na kuendesha gari akiwa amelewa, mwaka 2007 aliwahi kufungwa jela kwa muda wa siku tisini baada ya kupatikana na hatia ya kufanya fujo.Kutokana mwendo wa tabia zake kuwa tofauti na jamii iliyostarabika, Lindsay anapata ushauri wa kuacha kutumia dawa za kulevya.

Navuta majani- Tonto Dikeh

                                                                   Tonto Dikeh
Lagos Nigeria
Nyota wa sinema za Nollywood, Tonto Dikeh ameendelea na tabia yake ya kufanya vituko, ila kituko cha safari hii kimetokea kuwashangaza wengi waliopita mtandao na kuona amebandika picha ya bangi iliyokuwa na maneno ya kusifia kilevi hicho.
" Mimi navuta ganja, mimi navuta majani napata stimu wakati wengine wanavuta majungu," aliandika ujumbe kwenye picha hiyo bila ya kuwa na wasi wasi licha ya kilevi hicho kupigwa maarufu na serikali za nchi mbali mbali duniani.
Licha kutundika picha inayonyesha bangi na kuandika ujumbe wa kusifia, ametundika picha yake inayomuonyesha akiwa tayari amepata stimu, yaani amevuta bangi. Sura yake inaonyesha jinsi alivyokolea na kilevi hicho.

Flora Mvungi amefunga na H. Baba

Baada ya kuvuka mito, milima na mabonde hatimaye wasanii wawili wa fani tofauti, Hamisi Ramadhani a.k.a H Baba ambaye ni mwanamuziki wa miondoko ya tekeu na mwigizaji nyota wa sinema za kibongo maarufu kama Bongo Movie Flora Mvungi  weekend hii waliamua wakate vilimi vya watu wanaongea mjini na kufanikiwa kutimiza ahadi yao ya kufunga ndoa.
Wote  waliokuwa wakisema kama wawili hao hawataweza kufunga ndoa wamebaki kimya wakishindwa kuamini macho na masikio yao.
                                                            Flora akisaini hati ya ndoa
                                                                Flora akiwa katika send off yake

Friday, March 29, 2013

Teknolojia yapunguza kasi ya soko la sinama

Kukua kwa teknolojia kumechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kasi ya usambazaji wa kazi za sinema. Ikilinganishwa na zamani kabla ya Tanzania kukua katika teknolojia. Kwa mujibu wa maelezo ya Abdalah Shaban anayemiliki duka la jumla la kuuza VCD, DVD, VCD na CD, amesema kasi ya kununua TAPE, DVD, VCD au CD za muziki na sinema kama ilivyokuwa zamani imepungua sana. Shaban amesema hivi sasa watu wengi wanaweka sinema na nyimbo kwenye flash Disc. Kwa mfumo huo umuhimu wa TAPE, DVD, VCD na CD hakuna tena, hivi sasa TAPE zimeshaanza kupotea katika soko la muziki kama zilivyopotea VHS. “Nakaa dukani toka asubuhi mpaka jioni, nauza CD hamsini. Zamani nilikuwa nauza VCD elfu tatu mpaka tano. DVD elfu sita mpaka kumi. Wateja wengi wanaoingia dukani kwangu hivi sasa wanaulizia memory card na flash disc." Alisema Shaban. Majumbani kumejaa deki zenye kutumia memory card na flash disc Kwa mfumo huo hakuna mtu atakayenunua DVD, VCD na CD. Shaban amesema hatuwezi kukataa maendeleo ya kupanuka kwa teknolojia, ila tunatakiwa kuandaa mazingira ya kutumia teknolojia hiyo bila ya watu wengine kuumia. Hivi sasa wanaoumia na kuteseka na njaa ni wanamuziki na waigizaji, wanaofaidika ni wale wafanyabishara, wanaokaa vibarazani na Computer wakiweka nyimbo na sinema kwenye flash disc na memory card bila ya ridhaa ya waigizaji na wanamuziki wenyewe. Shaban anasema memory card na flash disc ziendelea kuingia nchini kwa sababu zina matumizi mengi zaidi ya kuweka nyimbo na sinema. Ila wangepiga maarufu uingiaji wa deki na redio zinazotumia memory card na flash disc. Wakifanya hivyo soko la DVD, VCD, CD linaweza kurudi kama mwanzo. Vinginevyo wasambazaji wa muziki na wauzaji wa jumla na rejareja wataacha na kuanzisha biashara nyingine zenye wateja.

Wema na Jaquliane mfano wa kuigwa

Aliyewahi kuwa Miss Tanzania na mwigizaji maarufu nchini, Wema Sepetu amefanya tukio la kistarabu baada ya kumsaidia mwigizaji mwenzake Kajala Masanja kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mitano baada ya kumlipia milioni kumi na tatu. Kwa mujibu wa hukumu ya hakimu Sundi Fimbo wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Alimuhukumu Kajala kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya milioni kumi na tatu za kitanzania. Wema alijitokeza kulipa faini hiyo, Kajala akajikuta akiwa uraiani akiwa huru. Mumewe alikosa mtu wa kumlipia faini alikuja akienda jela kutumikia kifungo. Kitendo alichofanya Wema Sepetu kinafanana na kile alichofanya mwigizaji mwingine maarufu anayeitwa Jaquline Wolper kwa kutoa kiasi kikubwa fedha kusaidia matibabu ya marehemu Sajuki. Waigizaji hawa ni mfano mzuri wa kuigwa, licha ya mapungufu yao. Kila binadamu ana mapungufu yake, cha muhimu kujiuliza yale mapungufu yao yanawaumiza wengine. Kama jibu hapana hatuna haki ya kuwasakama. Tunatakiwa kuwapa moyo ili waweze kuendelea kusaidia wenzao, kutoa msaada sio suala la kuwa na fedha nyingi. Wapo watu wana fedha nyingi sana lakini hawatowi msaada kwa mtu yoyote. Tukubali tusikubali Wema na Jaquliane ni mfano wa kuigwa. mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Wema na Jaquliane wanastahili pongezi. Kama kweli walichofanya Wema na Jaquliane ni kitu cha kawaida, hawastahili kupongezwa. Mbona hatujaona kampuni yoyote ya usambazaji wa sinema kutoa kiasi kikubwa cha fedha kama hicho kuwasaidia wahusika. Wakati wao wana fedha nyingi kuliko Wema na Jaquliane, swali kwenu.

Unamfahamu Angelina Jolie wa Tanzania

Angelina Joel mwenyewe wa Majuu Kama humjui Angelina Jolie wa Tanzania, kuanzia sasa unatakiwa kumfahamu kuwa ni Irene Paul. Mwigizaji anayekuja juu sana katika ulimwengu wa sinema za kibongo. Udhibitisho kama anakuja katika uigizaji. Unaweza kumwangalia katika sinema ya The Morning Alarm aliyocheza na Marehemu Steven Kanumba na Abdul Ahmed maarufu kama Ben. Stori imetungwa na Mtitu G Game. Script imeandikwa waandishi wa wawili, Haji Dilunga na Ally Yakuti. Baada ya kushiriki kucheza sinema za watu, hivi sasa Irene Paul ametayarisha sinema yake mwenyewe inayoitwa Kalunde. Ukipata DVD yake unaweza kumshuhudia Angelina Jolie wa bongo. Iren Paul a.k.a Angelina Joel wa bongo

Tuesday, March 26, 2013

Wema amnusuru Kajara kwenda Jela

HUKUMU ya kesi iliyokuwa inamkabili staa wa filamu za Kibongo, Kajala Masanja na mumewe imetolewa na Hakimu Sundi Fimbo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar. Katika hukumu hiyo Kajala amehukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi milioni 13 na mumewe kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi milioni 213. Kajala alikuwa anakabiliwa na kesi ya kuuza nyumba iliyowekwa kizuizini na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya mumewe, Faraji Agustino kukumbwa na msala wa kutaka kujipatia fedha haramu. Hata hivyo msanii Wema Sepetu amemwokoa Kajala kwa kumlipia faini ya shilingi milioni 13 ili kumnusuru na kifungo cha kwenda jela

Wema anawaongoza waigizaji wa kike

Baadhi ya wadau wa sinema wamesikika wakisema Wema Sepetu ni miongoni mwa waigizaji wanaopenda kuvaa viatu virefu kwa muda mrefu kuliko waigizaji wote wa kike. Mabishano hayo yalitokea kwenye baa moja maarufu wakati wakiangalia sinema ya DJ BEN iliyochezwa na Jacob Stephen, Irene Uwoya na Wema Sepetu. Jamaa mmoja iliyoonekana kulewa ilisikika ikiongea kwa sauti, Wema anaongoza kwa kuvaa viatu virefu. Kila utakapomuona iwe kwenye televisheni, magazeti au mtaani utamuona amevaa kiatu kirefu tofauti na waigizaji wenzake wa kike. “ Ni kweli Wema anapenda kuvaa viatu virefu, ila atakuja kulia uzeeni. Miguu itamsumbua sana." alidai mwanamke mmoja aliyekuwa akipata ulabu katika baa hiyo. “ Wema anaongoza wenzake, wapili nani na mwisho ni nani?" Aliuliza Mzee mmoja wa makamu huku akicheka kilevi. “ Wa pili Lulu," Mlevi mwingine alijibu.“ Sio Lulu, yule mke wa Ndikumana." mwingine alijibu. “ Anaitwa Irene Uwoya." Alijibu huyo Mwanamke. Shangazi Ezekiel akimanisha Auntie Ezekiel na Mrs Dallas akimanisha Jaquline Wolper mbona mmewasahau?" Yule Mzee wa makamu aliuliza. Jamaa aliyeanzisha mada hiyo alidai wiki ijayo wakikutana hapo atawatajia wa pili na mwisho. Swahilicinemanews tunakubalina na wadau kama mwanamke akivaa kiatu kirefu anapendeza. Kazi kwenu waigizaji wa kike kutinga viatu virefu kwa ajili ya kuvutia machoni mwa mashabiki wenu.

Waigizaji walia na serikali

Waigizaji wa sinema nchini, wametoa kilio chao kwa kuitaka serikali kuwasaidia kupata vitendea kazi ili kuleta uhalisi katika sinema zao na kutoa ushindani katika soko la kimataifa. Wamedai hivi sasa sinema zinapoteza uhalisi kwa sababu ya kukosa sehemu husika za kuigiza, mfano hai ni kukosekana kwa mavazi ya halisi ya Polisi, Jeshi, Trafik na Askari magereza, kuna changia sinema kupotea uhalisi. Mahitaji wanayotaka serikali kuwasaidia kuweza kupata kirahisi ni pamoja na mavazi ya askari wa aina zote, kutumia vituo vya polisi, majengo ya mahakama, bastola na bunduki, bendera, majengo ya hospital za serikali sambamba na majengo na maofisi ya serikali. Wameitaka serikali kuweka utaraibu wa kuwakodisha waigizaji ili kuweza kufanya maigizo yao katika ubora na uhalisi tofauti na hivi sasa.

Monday, March 25, 2013

What Ever Film kunyanyua chipukizi



         Mwaila na wenzake katika  sinema ya Zungu la Unga

Kampuni ya kutayarisha sinema na usambazaji ya What Ever Film imepania kunyanyua waigizaji chipukizi kwa kuwashirikisha katika sinema watakazotayarisha hivi karibuni.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Hussein Mwaila amesema mbali wa kuwashirikisha katika sinema zao, pia watasambaza sinema za waigizaji chipukizi walizotayarisha wenyewe.

" Tunapokea sinema za watayarishaji chipukizi na kuzisambaza, vigezo vyetu ni sinema kuwa nzuri. Yaani stori ieleweke, waigizaji wacheze kwa uhalisi wa hali ya juu sambamba na ubora wa rangi na sauti. Ikifanikiwa vigezo hivyo tunaichukua na kuisambaza." Alisema Mwaila.

Hata hivyo amesikitishwa na baadhi ya makampuni yanayokataa sinema za waigizaji chipukizi kwa madai kwamba haziuzi, kitu ambacho si kweli.

" Unajua kuna baadhi ya makampuni hayataki kuona vijana wapya wanachipukia kwa kuhofia mastaa wao waliongia nao mikataba wanaweza kufunikwa na waigizaji wanaochipukia. Hiyo ndiyo sababu ya kudai sinema walizocheza chipukizi haziuzi." Alisema Mwaila.

Alitoa mfano wa sinema ya kisiwa cha wachawi iliyochezwa na waigizaji chipukizi, inafanya vizuri sokoni mpaka sasa. Wakati zile sinema zilizochezwa na mastaa zinafanya vibaya.

Ukitaka kupata uthibitisho wa hiki ninachokueleza pita kwenye mabanda ya video, utagundua ukweli wa hiki ninachokueleza. Sinema nyingi za mastaa zinapowekwa watazamaji wanazomea na kutaka zitolewe, ila zinapowekwa sinema za waigizaji wanaochipukia wanashangilia kuzifurahia.

Kwa utafiti mdogo kama huo unaweza kupata taswira ya ukweli wa madai ya baadhi ya makampuni kwamba sinema za waigizaji wanaochipukia haziuzi.

Mwaila amesema What Ever Film watahakikisha dhana hiyo wanaitokomeza kwa wasambazaji wa jumla na rejareja kwa ajili ya kuwasaidia waigizaji chipukizi.