Monday, March 25, 2013

What Ever Film kunyanyua chipukizi



         Mwaila na wenzake katika  sinema ya Zungu la Unga

Kampuni ya kutayarisha sinema na usambazaji ya What Ever Film imepania kunyanyua waigizaji chipukizi kwa kuwashirikisha katika sinema watakazotayarisha hivi karibuni.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Hussein Mwaila amesema mbali wa kuwashirikisha katika sinema zao, pia watasambaza sinema za waigizaji chipukizi walizotayarisha wenyewe.

" Tunapokea sinema za watayarishaji chipukizi na kuzisambaza, vigezo vyetu ni sinema kuwa nzuri. Yaani stori ieleweke, waigizaji wacheze kwa uhalisi wa hali ya juu sambamba na ubora wa rangi na sauti. Ikifanikiwa vigezo hivyo tunaichukua na kuisambaza." Alisema Mwaila.

Hata hivyo amesikitishwa na baadhi ya makampuni yanayokataa sinema za waigizaji chipukizi kwa madai kwamba haziuzi, kitu ambacho si kweli.

" Unajua kuna baadhi ya makampuni hayataki kuona vijana wapya wanachipukia kwa kuhofia mastaa wao waliongia nao mikataba wanaweza kufunikwa na waigizaji wanaochipukia. Hiyo ndiyo sababu ya kudai sinema walizocheza chipukizi haziuzi." Alisema Mwaila.

Alitoa mfano wa sinema ya kisiwa cha wachawi iliyochezwa na waigizaji chipukizi, inafanya vizuri sokoni mpaka sasa. Wakati zile sinema zilizochezwa na mastaa zinafanya vibaya.

Ukitaka kupata uthibitisho wa hiki ninachokueleza pita kwenye mabanda ya video, utagundua ukweli wa hiki ninachokueleza. Sinema nyingi za mastaa zinapowekwa watazamaji wanazomea na kutaka zitolewe, ila zinapowekwa sinema za waigizaji wanaochipukia wanashangilia kuzifurahia.

Kwa utafiti mdogo kama huo unaweza kupata taswira ya ukweli wa madai ya baadhi ya makampuni kwamba sinema za waigizaji wanaochipukia haziuzi.

Mwaila amesema What Ever Film watahakikisha dhana hiyo wanaitokomeza kwa wasambazaji wa jumla na rejareja kwa ajili ya kuwasaidia waigizaji chipukizi.


No comments:

Post a Comment