Thursday, July 18, 2013

Danny Schechter ameitangaza Tanzania kwenye Movie ya Mandela

                                                                              
                                                                     Danny Schechter
Danny Schechter  a.k.a The News Dissector kwa wale wasio mfahamu ni mtayarishaji  kama sio mtengenezaji wa sinema ya Nelson Mandela – “Countdown to Freedom” na “Mandela in America” ametaka dunia kuiheshimu Tanzania kwa nafasi yake kubwa kwenye kutengeneza demokrasia Afrika Kusini.
Schechter anayefanya dokumentari ya utengenezaji wa filamu ya Long Walk to Freedom kama alivyotakiwa na Nelson Mandela mwenyewe, alisema Tanzania ilitoa ushirikiano mkubwa kukomboa mataifa mengi ya Afrika ikiwemo Afrika Kusini.
Jumapili katika Tamasha la ZIFF ilikuwa ni siku ya kuangalia Afrika Kusini kabla na baada ya Uhuru. ZIFF iliweka siku maalumu ya Afrika Kusini kutokana na maendeleo ya hali ya afya ya Nelson Mandela ambayo sasa inazungumzwa duniani kote.
Mandela ambaye katika dokumentari hiyo anaonekana akifafanua vitu mbalimbali, alielezwa na Schechter kama mtu maarufu ambaye hakutaka kuitwa mtakatifu pamoja na kwamba aliombwa kutengenezewa sanamu na kuwataka wasifanye hivyo na badala yake kusaidia ujenzi wa zahanati.
Alisema dunia inapaswa kutambua kwamba katika ukombozi wa Afrika Kusini, Tanzania ni nchi muhimu ingawa dunia inaonekana kutotambua hilo lakini wenyewe wa Afrika Kusini wanafahamu.
Alisema baada ya kuwapo na nia ya kutengeneza filamu yake, Madiba alimwandikia barua ya kumtaka kutengeneza dokumentari inayohusu utengenezaji huo kwa kuhakikisha ukweli uliopo kama unazingatiwa.
Alisema hali hiyo ilimfanya kufika Tanzania japo alishawahi kufika wakati wa harakati za ukombozi. Schechte ambaye ni mwandishi wa habari za uchunguzi, mtengeneza sinema huru, bloga na mhakiki vyombo vya habari, alisema ni vyema dunia ikatambua mchango wa Tanzania kwa ukombozi si wa Afrika Kusini, bali na mataifa mengine ya Afrika.
Alisema pamoja na utawala wa Makaburu kuzishambulia nchi zilizokuwa zinasaidia ANC kama Zimbabwe, Msumbiji, Angola na Zambia, ilishindwa kufanya hivyo kwa Tanzania ambayo licha ya kuwa na makambi ya mazoezi ya kivita, pia ilikuwa na shule za kufunza viongozi wa baadaye wa Afrika Kusini, Morogoro.
Dukumentari hiyo yenye tofauti kubwa na zile zinaozotengenezwa kwa ajili ya kuoneshwa katika televisheni, inamweleza Mandela kama mtu wa watu huku waliohojiwa wakielezea matumaini na nini kinafanyika.

No comments:

Post a Comment