Steven Kanumba
Kitendo cha baadhi ya wananchi kutumia jina la msanii aliyefariki kujipatia kipato au umaarufu ni kitu kibaya, kinachotakiwa kupigwa marufuku na kuwakamata wahusika na kufikisha mbele ya vyombo vya sheria.
Swahili Cinema News imeshuhudia mtu anayejiita Mchungaji George Kairuki akitumia jina la Marehemu Steven Kanumba kujipatia umaarufu katika kiwanja kilichokuwa Buguruni chama karibu na shule ya msingi, pamoja na kituo cha basi.
Mchungaji huyo aliibuka mara baada ya kifo cha Marehemu Kanumba na kueleza kama marehemu alikuwa muumini wa Freemasons, madai ambayo hakuna aliyekuwa na uhakika nayo.
Hata hivyo, kwa akili za kawaida madai hayo kwa sasa hayana umuhimu wowote, hakuna aliyetaka kufahamu kama alikuwa muumuni wa Freemasons. Kwa sababu haisaidi chochote hata watu wakifahamu.
Kikubwa anachofanya mchungaji huyo ni kujitafutia umaarufu kupitia mgongo wa marehemu Kanumba, taarifa ambazo kwa upande mwingine zilionyesha kumjenga kwa kumpatia umaarufu ili watu wajiunge na kanisa lake.
Kama lengo ni kutoa taarifa za Kanumba kujiunga na Freemasons, alikwishatoa baada ya kifo chake, vyombo vya habari viliandika na kutangaza.
Kwa hiyo hakuwa na sababu ya kuendelea kueleza taarifa hizo kwenye viwanja vya wazi. Ukifuatilia matukio ya mchungaji huyo, utagundua anachofanya ni kujitafutia umaarufu, mwaka jana alijisingizia kifo kilichofanana na kifo cha Marehemu Kanumba, magazeti ya udaku yaliandika taarifa zake na kuonyesha picha aliyokuwa kwenye jeneza.
Baada ya muda mfupi aliibuka kiwanja cha Buguruni akitoa maelezo ya namna Kanumba alivyokufa. Mchungaji huyu ni hatari anayestahili kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Wadua, Shirikisho, Familia na marafiki wa marehemu jitokeni kumtia adabu mtu huyo anayeendelea kujipatia umaarufu sambamba na kipato kupitia jina la Kanumba. Kwani hawezi kuzungumzia Freemasons bila ya kutaja jina la marehemu Kanumba.
Ikiwa nia yake ni safi, angeelezea imani ya Freemasons kwa kumtaja aliyekuwa kiongozi wa Afrika Mashariki, Sir Andy Chande , sio vizuri kumtaja mtu aliyekufa ambaye hawezi kujitetea.
Kwa mujibu wa maelezo yake anadai alikuwa anajua kama Kanumba ni muumini wa Freemasons kabla ya hajafa. Kama ni kweli, kwanini alikaa kimya mpaka alivyokufa na kuibuka kuanza kuzungumza mambo ambayo hayana faida kwa jamii. Badala yake ni kuhamasisha jamii ya vijana kutaka kujiunga na imani. Sisi wana Swahili Cinema News tunasikitishwa na tabia ya mchungaji huyo.