Monday, February 11, 2013

Sinema Tanzania, Inakuwaje movie zake kuwa na majina ya kizungu


Wapenzi na mashabiki waliobahatika kuongea na mtandao wa Swahili Cinema News, wamesema sinema za kitanzania kuwa na majina ya kizungu, ni ushamba na ulimbukeni wa hali ya juu.

“ Binafsi yangu sijawahi kuona sinema ya kihindi yenye jina la kizungu, au sinema ya kichina, Kijapan na kiarabu  zenye majina ya kizungu. Kama zipo itakuwa na jina la kizungu na jina la lugha yao" alisema Joshua Daniel.

Bi Sauda Ramadhani amesema sinema zilizotoka mwanzo zilikuwa nzuri, zilizingatia maadili ya kitanzania kuanzia stori, uvaaji, uchezaji na jina la sinema kuwa katika lugha ya kiswahili.

Alizitaja sinema hizo ni Nsyuka, Fungu la kukosa, Ngome ya Mwanamalundi, Lazima ufe Joram, Mambo ya ngoswe na nyingine nyingi za wakati huo.

“ Baada ya kuingia watayarishaji wanaopenda kuona mapaja ya watoto wetu wa kike, wakabadili mfumo wa utengenezaji sinema kwa kuandika majina ya kizungu.Kuwavisha nguo za ajabu mabinti wetu na kuwalazimisha kupigana mabusu, yaani huwezi kuangalia na watoto zako." Alisisitiza Bi Sauda.

Jaffar amesema kabla ya kina Ray, Tino, Johari, Mainda, Teya, Tito, Swebe, Maya, Zawadi, Nora, Nina na wengine, hawajaanza kuigiza sinema.

Walikuwa wakizingatia maadili katika michezo yao ya kwenye televisheni. Baada ya kuanza kujiunga na makampuni ya kutayarisha sinema, walibadilika kimaadili na kuanza kuvaa taswira ya kishetani. Taswira iliyowachukiza watazamaji wao.

“ Binafsi nilichukizwa na muonekano wao mpya, kwanza walikuwa wanaiga maadili ya kinaigeria kuanzia stori mpaka uchezaji." Alidai Jaffar.

No comments:

Post a Comment