Tuesday, February 19, 2013

Movie Tanzania, Inawezekana kila mwigizaji kutayarisha sinema?

  Inawezekana kila mwigizaji kuwa mtayarishaji wa sinema. Jibu linaweza kuwa ndio au hapana, kwa sababu utayarishaji wa sinema unaweza kufanywa na mdau yoyote mwenye uwezo wa fedha, ila awe anajua sanaa ya sinema kwa undani zaidi. Vinginevyo anaweza kuingia mikononi mwa wababaishaji na kujikuta akipoteza muda na fedha.

Mwigizaji anaweza kutayarisha sinema ila ni lazima awe na upeo mkubwa wa kutayarisha sio kuigiza, unaweza kuwa mwigizaji mzuri lakini ukashindwa kuwa mtayarishaji au muongozaji mzuri yaani director mzuri.

Wapo madirector wazuri sana, lakini hawawezi kuigiza. Kwa sababu hawana taranta au tunaweza kuita kipaji, wapo waandishi wazuri wa hadithi na vitabu, lakini hawawezi kuandika script.

Wapo wachezaji wazuri wa soka lakini hawezi kuwa makocha wazuri, wapo makocha wazuri lakini hawakuwahi kucheza mpira kwa kiwango cha kuitwa mastaa. Kwa hiyo ni vizuri kujikagua kama una taranta kabla ya kufanya chochote unachotaka kufanya.

Wapo waigizaji wenye taranta ya kutayarisha sinema na kuziongoza vizuri, mfano mwigizaji Mel Colm Cille Gerard Gibson wa Marekani, wengi wanamfahamu kwa Mel Gibson ni mwigizaji, mtayarishaji, mwandishi wa script na muongozaji. Moja ya sinema aliyoongoza ni Apocalypto

Marekani na Ulaya wapo wengi wenye uwezo wa kufanya yote katika utengenezaji wa sinema, pia wapo ambao hawawezi. Wanatoa nafasi kwa wenzao wanaoweza.
Kwa Tanzania hali ni tofauti, wengi hawawezi kutayarisha sinema wala kuziongoza. Ila wanajilazimisha kufanya hivyo kwa sababu wanajiona mastaa, ukweli unabaki kama sinema wanazotayarisha zinakuwa hazina ubora unaotakiwa.

Ukijiona huna uwezo wa kuandika script, kutayarisha na kuongoza. Tafuta wadau wenye uwezo wa kufanya kazi hizo kwa ajili ya kupata sinema nzuri. Matokeo ya kila kitu kutaka kufanya mwenyewe ni kutayarisha kazi mbovu.

Aliyekupa fedha za kutayarisha sinema akigundua sinema yako haipendwi na watazamaji, atakumwaga na hatimaye kupotea katika soko la sinema kabisa.

Kama lengo la wadau ni kuendeleza sekta ya uigizaji, waigizaji wanaopata bahati ya kuingia mikataba na wasambazaji kwa ajili ya kutayarisha sinema, wasiwe wabinafsi. Kuendekeza ubinafsi ni kuua sekta sinema, inayoongoza hivi sasa kwa kutoa ajira kwa vijana na wazee.
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment