Friday, November 28, 2014

Kidawa ni sinema yenye mazingira ya uswahili kikweli kweli

                                                  Nuru Mohamed a.k.a Kidawa
                                                                Mohamed Nurdin
                                                      Haji Adam  na Mohamed Nurdin
                                                               Haji Adam
                                                              Zainabu Mshindo

Katika makala yetu ya Sinema , leo naiangalia Sinema  inayoitwa Kidawa Uswahilini. Iliyotayarishwa na kampuni ya  Kapelele ya jijini Dar es Salaam na kusambazwa na kampuni ya BMO, pia  ya jijini Dar es Salaam. Ni filamu nzuri inayoelezea  vituko na visa vya wakazi wa maeneo ya uswahilini, hasa wale wanaoishi katika nyumba za kupanga.
Kidawa uswahilini inamzungumzia mwanamke anayeitwa Nuru Mohamed aliyecheza kwa jina la Kidawa na rafiki yake  Zainabu Mshindo aliyecheza kwa jina la Cecy ,  Mohamed Nurdin aliyecheza kwa jina Faiza, Haji Adam aliyecheza kama Mwasa pamoja na wapangaji wengine.
Hadithi (Story):
Wazo la hadithi  lilikuwa zuri sana, liliangalia mazingira ya maisha ya kweli wa wakazi wa maeneo ya uswahili na vituko vyao. Umbeya, chuki, shida, wivu wa kimaendeleo, ugomvi, matusi, kusutana, vyote hivyo vilionekana katika hadithi hii.  Kitu ambacho kwa watu wanaoishi maeneo ya watu wenye uwezo ni nadra kushuhudia mambo kama hayo. 
Nuru au Kidawa amecheza kama mwanamke mkorofi anayegombana na wenzake kila wakati,  nyumba inakosa amani na furaha kutokana na tabia yake ya ukorofi.  Zainabu au Cecy  katika sinema hiyo amecheza kama  rafiki wa Kidawa, anayevutiwa na ukorofi anaofanya Kidawa.
Mashoga hao wawili wametokea kuwa kero kwa wapangaji wenzao ambao ni Haji Adam au Mwasa na  Mohamed Nurdini au Faiza pamoja na wapangaji wengine wanaoishi katika nyumba hiyo yenye idadi kubwa ya wapangaji.
Sinema inaanza kwa Kidawa kupigana na mpangaji mwenzake anayeitwa Mwajuma,  majirani wanajitokeza kuwatenganisha,  kidawa anaonekana kutokubali na kuendelea kutoa matusi. wakati hilo likiwa bado halijapatiwa ufumbuzi, Mickynessy Joseph  aliyecheza kwa jina la Sinai  anamkuta Kidawa na rafiki yake Cecy wanamsema dada yake anayeitwa Sina. Wanarushiana maneno machache yanayoashiria kutaka kuleta ugomvi.
Kabla ya kumalizika hilo, wapangaji wote wanakaa kikao kujadili suala la umeme, kabla ya kufikia mwaka wa kikao hicho. Kidawa anakivuruga kikao kwa maneno yake ya kashfa na matusi na kisha kuondoka zake,  akidai kwamba hawezi kuendeshwa na watoto.
Kidawa aliongea hivyo baada ya watoto waliokuwa katika kikao hicho kudai kwamba Kidawa na Jenga wanamatumizi mabaya ya umeme.  Jenga ana mafriji mawili, Kidawa anapitisha marundo ya nguo ya rafiki zake kupiga pasi.
Kauli hiyo inamchukiza Kidawa na kuondoka zake katika kikao hicho, rafiki yake Cecy ananyanyuka anamfuata huku akiwa anatoa maneno ya matusi kumwambia miongoni mwa watoto waliokuwa wakichangia katika kikao hicho. Kiujumla  sinema hiyo inaelimisha na kuburudisha.
Usaili (Casting )
Mtu aliyefanya usaili (Casting Director)  alifanikiwa kuchagua waigizaji waliofanikiwa kuzitendea haki nafasi zao walizopangiwa kucheza.  Kila mmoja amecheza kwa kiwango cha hali ya juu, pongezi kwa casting director kwa kazi nzuri aliyofanya.
Mavazi (Costumes)
Aliyepangwa kuhakikisha waigizaji  wanavaa nguo zinazoendena na wakazi wa mitaa ya uswahilini,  kila mwigizaji alivaa kulingana na nafasi yake aliyocheza. Wapo wale waliovaa na  na kuonekana ni miongoni mwa wenye maisha nafuu zaidi ya wenzao kama vile Sinai na dada yake Sina anayeishi na mume wa mtu anayeitwa Faiza ambaye ni Nurdini. Wengine walionekana  ni wale wenye maisha ya kawaida hata Televishana hawana wanaangalia katika vyumba vya wenzao.
Mapambo (Makeup)
Mtu wa mapambo alifanikiwa kuwapamba vizuri na kuonekana ni miongoni mwa waliofanikiwa kuvaa taswira ya wakazi wa mitaa ya uswahilini kwa namna walivyopambwa na kupambika.
Mandhari(Location)
Mtu aliyepewa jukumu la kutafuta mandhari (Location) alifanikiwa kutafuta nyumba yenye uwezo wa kuchukua wapangaji wengi kwa wakati mmoja. Ki kweli kabisa anastahili pongezi kwa kufanikiwa kutafuta nyumba inayochukua wapangaji wengi kama nyumba hiyo iliyotumiwa kuchezea sinema ya Kidawa uswahiini.
Mwanga: (Light)
Mshika taa aliweza kushirikiana  vizuri na camera man wake  kuhakikisha wanatoa picha zenye ubora mzuri, licha baadhi ya scene zilionekana kuwa na mwanga hafifu pamoja na ubora mdogo. Alipoulizwa camera man   anayejulikana kwa jina la Rajabu Ngatale aliyeshuti sinema hiyo alisema baadhi ya scene zilitoka hivyo kutokana na camera ya mwanzo waliyotumia ilikuwa ina matatizo ya kiufundi.
Sauti (Sound man)
Sauti katika sinema hii haikuwa nzuri  sana,  hasa zile scene za  nje zilikuwa zina mvumo wa upepo. katika scene za ndani kutlikuwa na tofauti kubwa ya mabadiliko ya sauti hasa inapoingia shot ya CU  yaani ya karibu sauti inasikika vizuri. Inapokuja shot ya mbali yaani Long shot sauti inakuwa ndogo.  Tatizo lilitakiwa kuwekwa sawa na mhariri aliyehariri sinema hiyo.
Mhariri (Editor)
Mhariri alijitahidi kadri ya uwezo wake, lakini alishindwa  kuweka sawa tatizo la sauti. wakati mwingine mhariri anatakiwa  kuwa makini na sauti, sinema bila ya kuwa ana sauti inayosikika vizuri inapoteza utamu wake hata kama itakuwa stori  nzuri.
Muongozaji (Director)
Katika sinema muongozaji ni mtu muhimu sana katika kuhakikisha sinema inatayarishwa katika ubora unaotakikana kulingana na hadithi husika kwa kulinda wazo la mwandishi au mtunzi, ukiangalia filamu hii script imetendewa  haki licha ya mapungufu madogo madogo yalijitokeza kutokana  na sababu za kiufundi. Kwa wasiobahatika kuiona waitafute kushuhudia ufundi wa waigizaji wa sinema hiyo. Kwa naishi hapa tukutane katika sinema nyingine ya wiki..

No comments:

Post a Comment