Friday, March 29, 2013

Teknolojia yapunguza kasi ya soko la sinama

Kukua kwa teknolojia kumechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza kasi ya usambazaji wa kazi za sinema. Ikilinganishwa na zamani kabla ya Tanzania kukua katika teknolojia. Kwa mujibu wa maelezo ya Abdalah Shaban anayemiliki duka la jumla la kuuza VCD, DVD, VCD na CD, amesema kasi ya kununua TAPE, DVD, VCD au CD za muziki na sinema kama ilivyokuwa zamani imepungua sana. Shaban amesema hivi sasa watu wengi wanaweka sinema na nyimbo kwenye flash Disc. Kwa mfumo huo umuhimu wa TAPE, DVD, VCD na CD hakuna tena, hivi sasa TAPE zimeshaanza kupotea katika soko la muziki kama zilivyopotea VHS. “Nakaa dukani toka asubuhi mpaka jioni, nauza CD hamsini. Zamani nilikuwa nauza VCD elfu tatu mpaka tano. DVD elfu sita mpaka kumi. Wateja wengi wanaoingia dukani kwangu hivi sasa wanaulizia memory card na flash disc." Alisema Shaban. Majumbani kumejaa deki zenye kutumia memory card na flash disc Kwa mfumo huo hakuna mtu atakayenunua DVD, VCD na CD. Shaban amesema hatuwezi kukataa maendeleo ya kupanuka kwa teknolojia, ila tunatakiwa kuandaa mazingira ya kutumia teknolojia hiyo bila ya watu wengine kuumia. Hivi sasa wanaoumia na kuteseka na njaa ni wanamuziki na waigizaji, wanaofaidika ni wale wafanyabishara, wanaokaa vibarazani na Computer wakiweka nyimbo na sinema kwenye flash disc na memory card bila ya ridhaa ya waigizaji na wanamuziki wenyewe. Shaban anasema memory card na flash disc ziendelea kuingia nchini kwa sababu zina matumizi mengi zaidi ya kuweka nyimbo na sinema. Ila wangepiga maarufu uingiaji wa deki na redio zinazotumia memory card na flash disc. Wakifanya hivyo soko la DVD, VCD, CD linaweza kurudi kama mwanzo. Vinginevyo wasambazaji wa muziki na wauzaji wa jumla na rejareja wataacha na kuanzisha biashara nyingine zenye wateja.

Wema na Jaquliane mfano wa kuigwa

Aliyewahi kuwa Miss Tanzania na mwigizaji maarufu nchini, Wema Sepetu amefanya tukio la kistarabu baada ya kumsaidia mwigizaji mwenzake Kajala Masanja kwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mitano baada ya kumlipia milioni kumi na tatu. Kwa mujibu wa hukumu ya hakimu Sundi Fimbo wa mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam. Alimuhukumu Kajala kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya milioni kumi na tatu za kitanzania. Wema alijitokeza kulipa faini hiyo, Kajala akajikuta akiwa uraiani akiwa huru. Mumewe alikosa mtu wa kumlipia faini alikuja akienda jela kutumikia kifungo. Kitendo alichofanya Wema Sepetu kinafanana na kile alichofanya mwigizaji mwingine maarufu anayeitwa Jaquline Wolper kwa kutoa kiasi kikubwa fedha kusaidia matibabu ya marehemu Sajuki. Waigizaji hawa ni mfano mzuri wa kuigwa, licha ya mapungufu yao. Kila binadamu ana mapungufu yake, cha muhimu kujiuliza yale mapungufu yao yanawaumiza wengine. Kama jibu hapana hatuna haki ya kuwasakama. Tunatakiwa kuwapa moyo ili waweze kuendelea kusaidia wenzao, kutoa msaada sio suala la kuwa na fedha nyingi. Wapo watu wana fedha nyingi sana lakini hawatowi msaada kwa mtu yoyote. Tukubali tusikubali Wema na Jaquliane ni mfano wa kuigwa. mnyonge mnyongeni haki yake mpeni. Wema na Jaquliane wanastahili pongezi. Kama kweli walichofanya Wema na Jaquliane ni kitu cha kawaida, hawastahili kupongezwa. Mbona hatujaona kampuni yoyote ya usambazaji wa sinema kutoa kiasi kikubwa cha fedha kama hicho kuwasaidia wahusika. Wakati wao wana fedha nyingi kuliko Wema na Jaquliane, swali kwenu.

Unamfahamu Angelina Jolie wa Tanzania

Angelina Joel mwenyewe wa Majuu Kama humjui Angelina Jolie wa Tanzania, kuanzia sasa unatakiwa kumfahamu kuwa ni Irene Paul. Mwigizaji anayekuja juu sana katika ulimwengu wa sinema za kibongo. Udhibitisho kama anakuja katika uigizaji. Unaweza kumwangalia katika sinema ya The Morning Alarm aliyocheza na Marehemu Steven Kanumba na Abdul Ahmed maarufu kama Ben. Stori imetungwa na Mtitu G Game. Script imeandikwa waandishi wa wawili, Haji Dilunga na Ally Yakuti. Baada ya kushiriki kucheza sinema za watu, hivi sasa Irene Paul ametayarisha sinema yake mwenyewe inayoitwa Kalunde. Ukipata DVD yake unaweza kumshuhudia Angelina Jolie wa bongo. Iren Paul a.k.a Angelina Joel wa bongo

Tuesday, March 26, 2013

Wema amnusuru Kajara kwenda Jela

HUKUMU ya kesi iliyokuwa inamkabili staa wa filamu za Kibongo, Kajala Masanja na mumewe imetolewa na Hakimu Sundi Fimbo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar. Katika hukumu hiyo Kajala amehukumiwa kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi milioni 13 na mumewe kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya shilingi milioni 213. Kajala alikuwa anakabiliwa na kesi ya kuuza nyumba iliyowekwa kizuizini na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) baada ya mumewe, Faraji Agustino kukumbwa na msala wa kutaka kujipatia fedha haramu. Hata hivyo msanii Wema Sepetu amemwokoa Kajala kwa kumlipia faini ya shilingi milioni 13 ili kumnusuru na kifungo cha kwenda jela

Wema anawaongoza waigizaji wa kike

Baadhi ya wadau wa sinema wamesikika wakisema Wema Sepetu ni miongoni mwa waigizaji wanaopenda kuvaa viatu virefu kwa muda mrefu kuliko waigizaji wote wa kike. Mabishano hayo yalitokea kwenye baa moja maarufu wakati wakiangalia sinema ya DJ BEN iliyochezwa na Jacob Stephen, Irene Uwoya na Wema Sepetu. Jamaa mmoja iliyoonekana kulewa ilisikika ikiongea kwa sauti, Wema anaongoza kwa kuvaa viatu virefu. Kila utakapomuona iwe kwenye televisheni, magazeti au mtaani utamuona amevaa kiatu kirefu tofauti na waigizaji wenzake wa kike. “ Ni kweli Wema anapenda kuvaa viatu virefu, ila atakuja kulia uzeeni. Miguu itamsumbua sana." alidai mwanamke mmoja aliyekuwa akipata ulabu katika baa hiyo. “ Wema anaongoza wenzake, wapili nani na mwisho ni nani?" Aliuliza Mzee mmoja wa makamu huku akicheka kilevi. “ Wa pili Lulu," Mlevi mwingine alijibu.“ Sio Lulu, yule mke wa Ndikumana." mwingine alijibu. “ Anaitwa Irene Uwoya." Alijibu huyo Mwanamke. Shangazi Ezekiel akimanisha Auntie Ezekiel na Mrs Dallas akimanisha Jaquline Wolper mbona mmewasahau?" Yule Mzee wa makamu aliuliza. Jamaa aliyeanzisha mada hiyo alidai wiki ijayo wakikutana hapo atawatajia wa pili na mwisho. Swahilicinemanews tunakubalina na wadau kama mwanamke akivaa kiatu kirefu anapendeza. Kazi kwenu waigizaji wa kike kutinga viatu virefu kwa ajili ya kuvutia machoni mwa mashabiki wenu.

Waigizaji walia na serikali

Waigizaji wa sinema nchini, wametoa kilio chao kwa kuitaka serikali kuwasaidia kupata vitendea kazi ili kuleta uhalisi katika sinema zao na kutoa ushindani katika soko la kimataifa. Wamedai hivi sasa sinema zinapoteza uhalisi kwa sababu ya kukosa sehemu husika za kuigiza, mfano hai ni kukosekana kwa mavazi ya halisi ya Polisi, Jeshi, Trafik na Askari magereza, kuna changia sinema kupotea uhalisi. Mahitaji wanayotaka serikali kuwasaidia kuweza kupata kirahisi ni pamoja na mavazi ya askari wa aina zote, kutumia vituo vya polisi, majengo ya mahakama, bastola na bunduki, bendera, majengo ya hospital za serikali sambamba na majengo na maofisi ya serikali. Wameitaka serikali kuweka utaraibu wa kuwakodisha waigizaji ili kuweza kufanya maigizo yao katika ubora na uhalisi tofauti na hivi sasa.

Monday, March 25, 2013

What Ever Film kunyanyua chipukizi



         Mwaila na wenzake katika  sinema ya Zungu la Unga

Kampuni ya kutayarisha sinema na usambazaji ya What Ever Film imepania kunyanyua waigizaji chipukizi kwa kuwashirikisha katika sinema watakazotayarisha hivi karibuni.

Akizungumza na gazeti hili, Mkurugenzi wa kampuni hiyo Hussein Mwaila amesema mbali wa kuwashirikisha katika sinema zao, pia watasambaza sinema za waigizaji chipukizi walizotayarisha wenyewe.

" Tunapokea sinema za watayarishaji chipukizi na kuzisambaza, vigezo vyetu ni sinema kuwa nzuri. Yaani stori ieleweke, waigizaji wacheze kwa uhalisi wa hali ya juu sambamba na ubora wa rangi na sauti. Ikifanikiwa vigezo hivyo tunaichukua na kuisambaza." Alisema Mwaila.

Hata hivyo amesikitishwa na baadhi ya makampuni yanayokataa sinema za waigizaji chipukizi kwa madai kwamba haziuzi, kitu ambacho si kweli.

" Unajua kuna baadhi ya makampuni hayataki kuona vijana wapya wanachipukia kwa kuhofia mastaa wao waliongia nao mikataba wanaweza kufunikwa na waigizaji wanaochipukia. Hiyo ndiyo sababu ya kudai sinema walizocheza chipukizi haziuzi." Alisema Mwaila.

Alitoa mfano wa sinema ya kisiwa cha wachawi iliyochezwa na waigizaji chipukizi, inafanya vizuri sokoni mpaka sasa. Wakati zile sinema zilizochezwa na mastaa zinafanya vibaya.

Ukitaka kupata uthibitisho wa hiki ninachokueleza pita kwenye mabanda ya video, utagundua ukweli wa hiki ninachokueleza. Sinema nyingi za mastaa zinapowekwa watazamaji wanazomea na kutaka zitolewe, ila zinapowekwa sinema za waigizaji wanaochipukia wanashangilia kuzifurahia.

Kwa utafiti mdogo kama huo unaweza kupata taswira ya ukweli wa madai ya baadhi ya makampuni kwamba sinema za waigizaji wanaochipukia haziuzi.

Mwaila amesema What Ever Film watahakikisha dhana hiyo wanaitokomeza kwa wasambazaji wa jumla na rejareja kwa ajili ya kuwasaidia waigizaji chipukizi.