Showing posts with label Bekitatu. Show all posts
Showing posts with label Bekitatu. Show all posts

Wednesday, February 4, 2015

Sinema ya Bekitatu yatoa watu machozi


Unaweza kuona kama hadithi ya kufikirika, lakini tukio hili limetokea katika banda la video la maeneo ya Mwanagati, wilaya ya ilala, jimbo la Ukonga. Baadhi ya watu waliokuwa wakiangalia sinema hiyo walijikuta wakitokwa na machozi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Kijana anayeonyesha video katika banda hilo, anayejulikana kwa jina Festo amesema alichukua DVD ya BEKITATU kwa kushawishiwa na muuzaji, hakutarajia kama itatokea kuwa nzuri kiasi cha kuvutia watu.
"Wengi wameingia katika banda langu kuangalia video ya Swagga ya JB, baada ya kumaliza kuonyesha sinema ya Swagga niliweka Bekitatu yenye waigizaji wanaochipukia, baada ya kuweka katika deki, baadhi  watu walinyanyuka na kutoka nje,  ila wengine waliendelea kuangalia." alisema.Baada ya kuanza sinema na kuonekana kijana akinyata  kwenda kubaka, vijana waliokuwa wanaangalia wakaanza kupiga makelele ya kushangilia, waliotoka nje wakaanza kurudi kuangalia. Kadri sinema ilivyozidi kuendelea watu walianza kuingiwa na huruma na kuanza kusifia kama waigizaji wamejitahidi.
"Binafsi sina kawaida ya kutokwa na machozi ninapoangalia sinema za kibongo. Ila Bekitatu ni sinema ya aina yake, unapoangalia huwezi kujua nini kitakachotokea mbele, kila hatua inakuvutia kutazama.
Kama kuna wanawake makatili, Rukia ni miongoni mwao, kwa upande wa Bekitatu amecheza vizuri sana, ameweza kupokea manyanyaso kwa kiwango cha juu kiasi cha kuwafanya watazamaji kumuonea huruma na hatimaye kutokwa na machozi. Vipande vilivyonipa machungu makubwa ni pale walipompiga kwa kumchangia, chakula chake kilipotiwa katika maji machafu, chungwa lake kukanyagwa na kulazimishwa kula. Nguo yake ilivyochomwa moto, alivyonyimwa mshahara wake, kukanyagwa na kiatu. Sehemu nyingine ni watoto wa Rukia walivyokuwa wanatapatapa kwa ajili ya sumu, Bekitatu alivyokamatwa, Rukia analilia watoto wake baada ya kugundua wamekufa. Nikitaja vipande vyote nitamailiza sinema, kipande kilichowachekesha watu ni kile cha kijiweni. Hasa yule kijana mchungaji alivyokuwa akichangia maongezi na wenzake." alisema Festo.

Tuesday, January 6, 2015

Picha za waigizaji waliocheza sinema ya Beki tatu



Hawa amecheza Bekitatu
Nurati amecheza Rukia
                                                                 Clemensia amecheza Leila

Rafael kama Polisi

Hassan kama Bakari
                                                                       Isaya  kama Iyama
Amecheza kama Bibi wa Bekitatu

Anna amecheza Nasra 
                                                           Mlekwa kama Mlinzi
 
Pascal kama Ramson
                                                                 Nurdin kama Jaffary
                                                                Joyce kama Joy
                                                           Kana kama Mlinzi











FILAMU YA BEKITATU kuingia sokoni hivi karibuni

                                                                  Posters ya Bekitatu

Kikundi cha Sun Shine Artists Theatre chenye makao yake makuu  Ilala, jijini Dar es Salaam, kimetayarisha sinema inayoitwa Bekitatu inayotarajia kuingia sokoni hivi karibuni.  Kwa mujibu wa maelezo ya mtayarishaji  wa sinema hiyo Haji Dilunga amesema Beki tatu inaelezea na kutoa taswira ya jamii ya kitanzania inavyoishi na wafanyakazi wa ndani. Ni sinema inayofichukua siri nzito ya maisha ya wafanyakazi wa ndani na mabosi zao.Katika sinema hiyo Mwanadada Nurati Ngeleshi amecheza kwa jina la Rukia,  akiwa na watoto zake ambao ni  Nurdin  Salum aliyecheza kama Jaffary.  Clemensia Salum aliyecheza kama Leila, Hassan Lukuu aliyecheza kwa jina la Bakari akiwa kama mdogo wake Rukia. Mwingine ni Hawa Hassan aliyecheza kwa jina Sikitu au Bekitatu, katika sinema hiyo  amecheza kama mfanyakazi wa ndani wa familia ya Rukia.  Sinema inafumbua fumbo la kwanini wafanyakazi wa ndani wanatokea kutenda vitendo vya kikatili kwa mabosi wao."Sidhani kama  wewe mpenzi wetu utakuwa unafahamu, jibu lake ni kutafuta sinema hiyo utafahamu kwanini wafanyakazi wa ndani wanatenda vitendo vya kikatili kwa mabosi zao. Ni sinema inayosikitisha na kuhudhunisha, wakati huo huo kufurahisha na kutoa elimu kwa jamii." alisema Dilunga.Sinema hiyo imetungwa na kuandikwa script na Haji Dilunga, inasambazwa na kampuni ya BMO ya jijini Dar es Salaam ,  kuikosa sinema hiyo ni sawa na kukosa kitu muhimu sana katika maisha.Kama unakumbukumbu ya sinema ya Kwanini Mama? Jamila na Pete Ajabu, Mwandishi, Sound of Death   na nyingine nyingi zilizoandikwa na Haji Dilunga.  Beki tatu ni miongoni mwa hizo au zaidi ya hizo kwa utamu wa stori na mtiririko wa visa.Usiogope kununua kwa vile imechezwa na waigizaji wachanga, ununu ili upate uhondo na kutambua uwezo wa waigizaji wanaochipukia katika ulimwengu wa sinema.wale wanaotaka nakala ya sinema yetu wasikose kupiga namba hizi 0753 833773 au 0655 833 772.

Sinema Bekitatu ni mwanzo mambo makubwa yanakuja- Leila



                                                                 Clemensia Salum
Clemensia Salum

MWIGIZAJI Chipukizi katika tasnia ya filamu bongo, Clemencia  Salum a.k.a Leila amejigamba kwa kusema kuwa pamoja na kuwa msanii chipukizi anaamini kuwa ataliteka soko la filamu na tasnia kwa ujumla kwa sababu amejipanga kufanya kazi  nzuri  iliweza kushindana na wakongwe waliotangulia katika gemu kabla yake.
Kwa mujibu wa maelezo yake, Leila  amesema  hakuna kitu anachopenda  katika maisha kama kuigiza.  Kitendo cha kuanza kuigiza ni kutimiza ndoto yake ya muda mrefu, kwa hiyo hana budi kufurahi kwa kufanikisha kutimiza yale alivyokuwa akiyafikilia kila siku katika maisha yake.
“Ninaamini kuwa haya ndio maisha yangu na ili niweze kudumu katika tasnia ya filamu ni lazima niwe makini, najua kila mtu kwa sasa anatamani kuigiza na kuwa nyota, kwa kuandikwa sana katika vyombo vya habari lakini kwangu si hivyo niandikwe kwa ajili ya kazi, nia yangu nikuwapoteza wakongwe wote waliopo katika sanaa,”anasema Leila.
Mwigizaji huyo mwenye umbo dogo lakini ni machachari katika kuigiza, amejikuta akifananishwa na  mwigizaji wa Nigeria mwenye umbo dogo kama yeye anayeitwa Genevieve Nnaji .
"Nafurahishwa kufafanisha na mwigizaji mkubwa kama Genevieve Nnaji, kwa sababu ni miongoni mwa waigizaji ninaowapenda sana na ninajifunza vitu vingi toka kwake. Kwa upande waigizaji wa Tanzania anavutiwa na Ndumbagwe Misayo a.k.a Thea." alisema Leila.
Mwigizaji  huyo aliyezaliwa Desemba 28 mwaka 1996,  wilaya  ya Urambo mkoani Tabora, alipata elimu ya msingi katika shule ya Azimio,  mwaka 2010  alijikutaka akimaliza elimu yake ya msingi. Kutokana na matatizo ya kifamilia alishindwa kuendelea na masomo ya sekondari.
Hata hivyo hakutaka kuongelea zaidi matatizo ya kifamilia, ila alisema baada ya kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari aliamua kuja jijini Dar es Salaam kwa mama yake Mzazi aliyekuwa tayari ameachana na baba yake.
Leila ni miongoni mwa wasichana wapambanaji au unaweza kuita ni miongoni mwa wasichana watafutaji, alivyofika jijini Dar es Salaam eneo la Vingunguti  anapoishi mama yake, akutaka kuwa golikipa wa kila kitu kutafutiwa na mama yake. Aliamua kutafuta shughuli za kufanya ili kujipatia kipato kitachomsaidia kuendesha maisha yake,
"Nimefanyakazi katika viwanda mbali mbali kama vile kiwanda cha kuteneneza vyombo vya plastic,  kiwanda cha kuteneneza Pipi,  kiwanda cha kutengeza mafuta ya kupikia, kiwanda cha kutengeneza kandambili, nimeuza duka la kuuza hina eneo la kariakoo na kutembea bidhaa za promosheni," alisema Leila.
Katika mahojiano na  gazeti hili,  Leila  anasema kwa vile sanaa ipo katika damu yake aliamua kutafuta kikudni cha kujiunga ili kuweza kujifunza mbinu mbali mbali za kuigiza na kufanyikisha malengo yake.
Miongoni mwa makundi aliyowahi kupitia ni pamoja na kikundi cha Dedede kilichokuwa Vingunguti, alifanya kwa muda mfupi na kuamua kuacha baada ya kugundua kikundi hicho hakina dira ya maendeleo zaidi ya kupotezeana muda.
"Kuna baadhi ya vikundi vinaanzishwa havina hata dira ya maendeleo, kila siku mnafanya mazoezi lakini hakuna cha maana mnachotarajia kufanya zaidi ya kupotezeana muda.  Utakuta katika kikundi  hakuna mtu mwenye taalamu ya kutayarisha tamthilia au sinema,  wote mliokuwa hapo ni sawa na wanafunzi wanatarajia kupata mwalimu wa kuwaelekeza," alisem,a Leila.
Baada ya kuachana na kikundi hicho alijikuta anajiunga na kikundi cha Alwatan cha Ilala na kubahatika  kushiriki katika sinema ya Sound of Soul. Katika sinema hiyo amecheza kama mzimu.
"Licha ya kucheza scene moja katika sinema hiyo, linaweza kuitendea haki scenem hiyo mpaka nikajikuta katika sinema nyingine iliyotengenezwa na kikundi cha Sun shine ambayo kinaongozwa na yule yule alyekuwa anaongoza kikundi cha Alwatan, alinipatia nafasi ya kubwa ya kushiriki katika Bekitatu, kusema sikumwangusha nimefanya vizuri sana. Namshukuru mungu,"alisema Laila.
Matarajio yake ni kuja kuwa mwigizaji wa maarufu wa kitaifa na kimataifa,  japokuwa wengine wanaona kama vigumu ila kwake anaamini hakuna kinachoshindikana. Kuweza kushiriki katika sinema ya Bekitatu kwa kucheza kama mshiriki mkuu,  akisaidiana na wenzake kama Hawa Hassan, Nuruti Ngeleshi, Nurdin Salum na Hassan Lukuu pamoja na wengine waliocheza kama  sapota.
Akielezea nafasi aliyocheza katika Bekitatu, amesema amecheza kama mtoto wa Nurati Ngeleshi ambaye ni Rukia,  anatokea kumchukia  mfanyakazi wao wa ndani,  Hawa Hassan aliyecheza kama Bekitatu.
Leila anadai kwamba alimchukia Bekitatu wao baada ya kugundua anatongozwa na kijana anayeitwa Ramson, yeye alitokea kumpenda huyo kijana. Hakutaka kushuhudia Ramson akiwa mpenzi wa mfanyakazi wao badala yake.
Kuanzia hapo akaanza kumfanyia vituko na visa vya aina mbali mbali huku mama yake akionyesha kama kuvutiwa na vitendo anavyofanya binti yake.
"Kusema kweli Bekitatu ni sinema nzuri sana watu wasikose kuinunua na kuiangalia, ina mafundisho mazuri kwa jamii yetu. Hata mavazi tuliyovaa ni mavazi ya heshima, hakuna mtu aliyevaa nusu uchi." amesema Leila.
Hata hivyo Leila amesema sinema hiyo imeandikwa stori na script na mtaalamu wa kuandika script zinazovutia, si mwingine ni Haji Dilunga.  Script nyingi alizoandika na kutengenezwa sinema zimetokea  kuvutia watu wengine sana. wale wanaotaka nakala ya sinema yetu wasikose kupiga namba hizi 0753 833773 au 0655 833 772.

Nurati aibuka ndani ya Sinema ya Bekitatu

                                                         
                                                                 
Nurati Ngeleshi


Nurati Ngeleshi
Mwigizaji anayechipukia katika ulimwengu wa sinema nchini,  Nurati Ngeleshi a.k.a Belinda ameitaka serikali kuwasaidia kurahisisha upatikani wa vitendea kazi ili kuleta uhalisi katika sinema zao, sambamba na kutoa ushindani katika soko la kimataifa.
Kwa mujibu wa maelezo yake,  Belinda  amesema sinema nyingi zinazotayarishwa hivi sasa, hazina ubora na uhalisia kwa sababu ya kukosekana vitendea kazi na sehemu husika za kuigizia.
Amesema inakuwa vigumu kupata mavazi ya kweli ya polisi, jeshi, magereza na trafiki. Kukosekana kwa mavazi hayo kunachangia sinema zetu kupoteza uhalisi.
“Hebu angalia sinema za waafrika wenzetu kama Nigeria, Ghana, Kenya, Uganda na nchi nyingine. Utaona walivyopiga hatua katika kujenga uhalisia wa sinema zao kwa kutumia vitendea kazi husika na maeneo husika ya kuigizia" alisema Belinda.
Serikali ingesaidia watayarishaji kupata kwa urahisi mavazi ya askari wa aina zote, kutumia vituo vya polisi, majengo ya mahakama, bendera, majengo ya hospital za serikali sambamba na maofisi yake.
Kwa upande wa silaha, serikali ingeruhusu  bastola, bunduki na hata mabomu ya bandia kuingia nchini kwa ajili ya kurahisisha utayarishaji wa sinema kwa lengo la kuleta uhalisia.
Hivi sasa wengi wanatayarisha sinema kwa kutumia vibastola vya kuchezea watoto. Mtu yoyote akitazama anagundua kama ni kibastola cha watoto, ubora unapungua na uhalisia unapotea.
Belinda amewataka baadhi ya wadau na viongozi wa serikali, wasipende kulalamika kama sinema za kitanzania hazina uhalisia, eti kwa sababu wanavaa nguo fupi na kucheza sana kuhusu mapenzi. Kabla ya kulalamika walitakiwa kuitazama jamii ya kitanzania, wanaweza kupata majibu ya kwanini watayarishaji wanatengeneza sinema za kuvaa vimini na mapenzi.
Kwa kawaida mtayarishaji, mwandishi wa kitabu au mtunzi wa nyimbo, wana kawaida ya kutunga au kutengeneza yale mambo yanayotokea katika jamii yetu. Sio rahisi kutunga vitu vya kufikirika.
Kwa hiyo vimini na mapenzi ndivyo vinavyoendelea hivi sasa katika jamii yetu. Ndio maana sinema zinahusu mapenzi, nyimbo zinahusu mapenzi na vitabu vinahusu mapenzi.
Belinda ameitaka serikali kuweka utaratibu wa kuwakodisha waigizaji vitendea kazi vitakavyosaidia kuleta uhalisia na ubora tofauti na hivi sasa. Hata hivyo serikali inatakiwa kujua kama sinema imetoa na kuendelea kutoa ajira kwa watu wengi nchini.
Akizungumzia  maisha yake ya sanaa, anasema alizaliwa wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro. Sanaa alianza kuifanya  toka alivyokuwa shule,  baada ya kumaliza hakuendelea na mambo ya sanaa zaidi ya kujitumbukiza katika biashara.  Alikuwa akitoka Rombo kwenye Kenya kufanya biashara.
"Si unajua toka Rombo kwenda Kenya ni karibu sana, kipindi kile vijana wengi walikuwa wanakwenda Kenya kufanya biashara, hivi sasa hali imebadilika vijana wengi wanatoka kenya kuja Tanzania kufanya biashara." alisema Belinda.
Anadai kwa vile sanaa ipo katika damu yake alivyokuja Dar es Salaam aliamua kujifunza kuandika script na kuhakiki, miongoni mwa sinema ambazo alihakiki ni pamoja na Uwanja wa dhambi,  I love you, Bunge la wachawi,  Picnic, Popobawa, Zindiko na sinema mpya ya Bekitatu.
"Kwa vile nilikuwa na kipaji cha kuigiza  nilijikuta nikikosa kila wakati ninapoangalia sinema,  nikaamua kujinga katika kikundi cha Alwatan Artstis Theatre kilichokuwa chini ya uongozi wa  mwalimu wangu wa script, Haji Dilunga.", alisema Belinda
Baada ya kujiunga na kikundi hicho alishiriki kucheza sinema inayoitwa Julio na Romeo iliyotungwa na kuandikwa script na Haji Dilunga, katika sinema hiyo alicheza kama dada anayesambaratisha penzi la mdogo wake kwa kumtafutia msichana mwingine.
 Mbali ya sinema hiyo, alipata nafasi ya kushiriki katika sinema nyingine iliyotungwa na kuandikwa script na Haji Dilunga, inayoitwa Sound of soul.
Katika hali ya kuleta ushindani na changamoto katika ufanisi, Dilunga aliamua kuanzisha kundi la jingine linaloitwa Sun Shine Artists Theatre kwa ajili ya kuleta ushindani miongoni mwetu. Kwa bahati nzuri nilijikuta nikiwa katika Sun shine badala ya Alwatan, waigizaji wengine niliocheza nao sinema hizo nilizotaja wamebaki katika kundi la Alwatan.
Maisha ya kifamilia nimeolewa, nina watoto wawili wa kiume. Nampende mume wangu na kuheshimu, mwigizaji anayenivutia ni kutoka Nigeria anaitwa Omotola Jalade Ekeinde .  Anavutiwa na namna anavyoigiza na mapozi yake.
Belinda amewataka wapenzi na mashaki wanunue sinema ya Bekitatu wajionee kile alichofanya, watakubaliana naye kwa sanaa ni kipaji nasio kulazimisha kama wengine.
Amesema katika sinema ya Bekitatu amecheza kama mwanamke anayeishi na mfanayakazi wa ndani anayeitwa Sikitu au Bekitatu, katika sinema hiyo anaonekana anavyomtesa mfanyakazi wake wa ndani.
"Ni sinema nzuri inayosikitisha, kufurahisha na kuelimisha, kuikosa ni dhambi kubwa kwa sababu utakuwa umekosa ujumbe muhimu sana katika maisha yako,"alisema Belinda.Wale wanaotaka nakala ya sinema yetu wasikose kupiga namba hizi 0753 833773 au 0655 833 772.